Thursday, August 11, 2016

UFUGAJI BORA WA KUKU WA KIENYEJI



Idadi ya wanyama wanaofugwa kwa chakula imezidi ile ya binadamu zaidi ya mara mbili kote ulimwenguni. Kuna maelfu ya wanyama kote duniani ilihali ni wachache tu wanaoweza kufugwa. Kati ya hawa wanyama, ni aina nne (Ng'ombe, kondoo, mbuzi na kuku) wanaochukua asilimia 95% ya wanyama wote wanaofugwa. Wanyama hawa hupatikana katika nchi za hari kwenye nyanda za chini. Lakini kati ya mifugo hawa, kuku ni maarufu katika nchi za hari na hata kote ulimwenguni.
Lengo la makala haya ni kutoa maelezo ili kusaidia wafugaji wa kiwango kidogo katika nchi
zinazostawi, katika kupunguza umaskini. Sehemu ya kwanza (I) itatoa maelezo kuhusu ufugaji na
hasa ufugaji wa kuku, Sehemu ya pili (II) itaangazia maswala yafuatayo katika kuinua hali ya uchumi
kwa kufuga kuku:
1. Kuendeleza ufugaji wa kuku za kienyeji kwa kutumia njia zisizohitaji gharama nyingi.
2. Kutafuta mbinu na njia muafaka za kuzalisha viwango vya kuku bora kwa njia ya kiasili.
3. Matumizi ya njia za kiasili au zile zisizo gharimu pesa nyingi kutibu na kuzuia magonjwa ya
kuku.

NAFASI YA MIFUGO

Licha ya kukosa mashamba makubwa ya kuendeleza ufugaji wa ng'ombe, jamii nyingi katika nchi za
hari (tropics) hupata nafasi ya kufuga kuku kwa kiwango kidogo. Idadi ya wanyama wanaofugwa
huongezeka sambamba na ile ya watu. Idadi ya watu inapoongezeka ndipo ile ya mifugo huzidi.
Idadi kubwa ya watu huhitaji chakula kingi na matumizi huongezeka, hivyo basi watu hufanya bidii
kuzalisha chakula na mapato kutoka kwa shamba.
Ufugaji wa ng'ombe na wanyama wanaohitaji lishe kwa wingi huhitaji kiasi kikubwa cha shamba ili
kupanda mimea na lishe la mifugo. Ukilinganisha na ufugaji wa kuku, utahitaji mabaki ya vyakula
na sehemu ndogo ya shamba. Ufugaji wa kuku umeweza kunawiri hata pasipo fedha.
Katika nchi za hari ufugaji wa kienyeji hautahitaji kazi nyingi, kazi hii hufanywa na akina mama na
watoto. Kwa kawaida katika nchi hizi kazi nyingi za nyumbani hutekelezwa na mama. Vyakula vya
kuku vyaweza kutoka kwa: 1) Mabaki ya chakula, 2) Mabaki ya mimea, 3) Mabaki kutoka jikoni
na 4) Vyakula vya kujitafutia (kwa mfano kwekwe, mbegu, wadudu, nyongonyongo, n.k). Mfumo
wa kufuga kuku kwa njia ya kienyeji hutumia viungo vinavyopatikana kwa urahisi na kuimarisha hali
ya kiuchumi na chakula bora kwa jamii.
Ni muhimu sana kufuga mifugo hata ikiwa ni kwa kiwango kidogo kwa sababu ya 1) Chakula bora
na kuongeza mapato ya jamii kwa viwango vya kuridhisha; 2) Mifugo ni hakiba au banki, faida yake
huzaana tu kama riba ya benki; 3) Mifugo yaweza kuuzwa ili kugharamia karo ya wanafunzi,
malipo ya hospitali, gharama nyingine za nyumbani na hata shambani; 4) Kwa matumizi ya kijamii
(kwa mfano kulipia mahari, shughuli za kidini, n.k); 5) Mifugo husaidia katika kukabili wadudu,
kwekwe na kuimarisha rutuba kutokana na mbolea ya kinyesi. Ni bayana kwamba mifugo ni
muhimu sana kwa mkulima yeyote yule.


UMUHIMU WA UFUGAJI WA NJIA YA KIENYEJI

Ufugaji wa kuku katika nchi zinazostawi waweza kugawanywa mara mbili: 1) Ufugaji wa
kitamaduni au kienyeji pasipo kuwepo gharama, na 2) Ufugaji wa kisasa unaohitaji fedha nyingi.
Ufugaji wa viwango vikubwa kwa kuzingatia mfumo wa kisasa ni maarufu katika kuzalisha kuku wa
nyama na wale wa mayai. Mfumo huu hujumuisha asilimia ndogo sana ya aina ya ufugaji.
Itafahamika kwamba mfumo wa kisasa haujaadhiri ule wa kienyeji. Idadi kubwa ya watu katika nchi
za hari hutegemea mfumo wa kienyeji kwa nyama na mayai.
Mfumo wa kisasa huhitaji pesa nyingi za kununua vyakula vya kuku. Aidha mfumo wa kisasa huhitaji kazi nyingi ili kutekeleza. Mfumo wa kisasa
umefaulu katika nchi zilizostawi kutokana na hali nzuri ya kiuchumi katika kuzalisha (kuku wa hali
ya juu, kuangua vifaranga kwa stima, vyakula vilivyo na madini mengi, vifaa na zana za mashine,
utaalamu wa hali ya juu n.k). Haitafaa sana kuanzisha mfumo kama huu katika vijiji vya mataifa
yanayostawi.
"Mageuzi" katika ufugaji (kuambatanisha mfumo wa kisasa pamoja na ule wa kienyeji) yamefanyiwa
majaribio katika mataifa yanayostawi tangu miaka ya 1950. Matokeo ya kuku wapatao 200 hadi 300
kwa shamba moja hayajawai kufaulu. Hasara imepatikana na waweza kuona nyumba zilizokuwa na
kuku bila chochote, pesa nyingi zimepotea na kuku hawapo.
Mfumo wa kienyeji ni bora (Katika hali ya kiuchumi) iwapo idadi ya kuku haitazidi kuku 50. Ni
rahisi kuweza kuwatunza kuku, kwani hakuna gharama nyingi. Iwapo vyakula au zana za kisasa
zitanunuliwa, basi haitakuwa kwa viwango vikubwa. Mazao ya nyama na mayai yataleta faida.
Sehemu nyingi katika mataifa yanayostawi hakuna stima, katika nchi za hari, ufugaji kwa kiwango
kidogo umeweza kufaulu na kuimarisha uchumi.


FAIDA ZA UFUGAJI WA KUKU KWA NJIA YA KIENYEJI

Faida za uzalishaji kuku ili kuimarisha uchumi kwa njia hii zimepuuzwa na viongozi na wafadhili.
Kuku huleta faida kwa jamii kama tulivyoona katika sehemu ya I. Zaidi ya hayo, ufugaji wa kuku waweza kuimarishwa pasipo gharama nyingi ukilinganisha na mifugo wengine.
· Hutupatia fedha kwa kuuza nyama na mayai
· Mayai ni chakula kilicho na madini muhimu na kisicho ghali katika soko lolote. (madini kama methionine na cystine), madini haya ni muhimu sana kwa afya ya watu hasa watoto wachanga. Pia hutupatia protini.
· Kinyesi cha kuku ni mbolea safi
· Kiwanda asilia cha kutotoa vifaranga
· Gharama za kuanzisha na kuendeleza ni nyepesi
· Kitoweo chepesi na rahisi kwa wageni, kitoweo hakihitaji hifadhi hutumika mlo mmoja au miwili na kumalizika
· Jogoo hutumika kama saa inapowika
· Manyoya ya kuku hutumika kutengenezwa mapambo mbalimbali, mito na magodoro
· Kuku wanahisimu wadudu waharibifu
Kuku ndiye mnyama wa kipekee anayeweza kuishi mahali popote hapa ulimwenguni bila kuadhiriwa
na viwango vya hali ya hewa. Ufugaji wa kuku ndio shughuli inayofanyika kwa wingi duniani kuliko ufugaji wa aina yeyote. Kuku hunawiri vyema katika nchi za hari kutokana na uwiano uliopatikana wakati wa mwanzo binadamu alipofuga Asian jungle fowl aina ya kuku-mwitu. Mayai pia yaweza kuhifadhiwa kwa urahisi na huchukua nafasi ndogo kuliko aina ya bidhaa zozote za mifugo. Mayai yaweza kuwekwa mahali kwa muda mrefu bila kuhitaji barafu. Hautahitaji kuhifadhi kuku kwa njia yoyote, kwani nyama yake hupatikana pale unapohitaji kwa kuchinja.

TEKELEZA UTARATIBU WA KUZUIA MAGONJWA

Magonjwa ndio husababisha hasara katika mfumo wa ufugaji wa kuku. Kuku waliochanjwa dhidi ya
magonjwa hudumisha afya bora. Jaribu kila mara kuzuia magonjwa, kwani kuzuia ni bora kuliko
kuponya. Kinga yaweza kutolewa mara kwa mara (kila baada ya miezi mitatu) dhidi ya magonjwa
yafuatayo:

Ugonjwa wa Newcastle

Ugonjwa huu ndio huadhiri kuku na kusababisha hasara katika nchi za hari. Virusi vya ugonjwa huu
huenea kwa kasi na rahisi kiasi cha kusababisha vifo kwa asilimia 100%. Dalili za kwanza ni shida
ya kupumua na kung'amua hewa, sauti kama ya kikohozi na kutokwa mate. Kinyesi chaweza kuwa
na rangi ya kijani kibichi. Hadi sasa hakuna dawa.
Waweza kuzuia ugonjwa huu kwa kutoa chanjo. Dawa za chanjo hupatikana kote ulimwenguni hata
katika nchi za hari kwenye vipimo vya vitone mia moja. Madawa haya yaweza kuhifadhiwa kwa
muda. Waweza kuweka kwa wiki moja mbali na jua au joto kali (Chanjo hii ni ya kipekee, kwani
aina nyingine ya chanjo huwekwa kwa friji). Waweza kutoa chanjo kwa kutia vitone kwenye
mdomo. Kuku wote (wakubwa kwa wadogo) wapaswa kupewa chanjo baada ya kila miezi mitatu.

Minyoo

Minyoo kama chango (roundworms) na tegu (tapeworms) huadhiri kuku wa kienyeji. Kuku hukosa hamu ya chakula, mayai hupungua na magonjwa mengine hushambulia. Ni bora basi kutoa minyoo.
Mchanganyiko wa madawa ya aina tatu ndio hutumiwa kuangamiza minyoo, madawa haya ni
piperazine, phenothiazine na butynorate. Madawa haya hupatikana kama vidonge (tumia kidonge 1
kwa kuku mzima na 1/2 kwa vifaranga). Iwapo hautapata dawa hii, waweza kutumia Panacur au
dawa nyingine ya kuangamiza minyoo. Wapatie kuku dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu.

Wadudu

Wadudu kama chawa au utitiri husumbua kuku katika ufugaji wa kienyeji. Chawa au utitiri
husababisha harara ya ngozi, kuku walio adhiriwa hupata shida na kukosa usingizi. Hali hii
hupunguza kiwango cha mayai na uzito wa kuku.
Tumia asilimia 5% ya unga wa malathion kwa kupulizia kuku (puliza kwa chupa uliyo toboa
mashimo) pulizia kila kuku ili kuzuia chawa na utitiri (kilo moja ya unga huu yaweza kutibu kuku
150). Pulizia dawa hii baada ya kila miezi mitatu, waweza kupuliza kwa wakati mmoja wa kutoa
chanjo na dawa zilizotajwa hapo juu. Puliza unga huu pia kwenye viota vya kuangulia mayai.
Waweza kutayarisha 5% ya malathion kwa kuchanganya 25% ya unga wa malathion (kiwango cha
kilimo) na sehemu nne za jivu kutoka jikoni.

Magonjwa ya mapafu

Magonjwa ya mapafu huadhiri njia inayopitisha hewa na kuambatanisha mate na sauti kama ya
kikohozi. Ugonjwa huu huenea polepole. Uambukizanaji pia hutokea kwa polepole na vifo sio kwa
wingi. Hata hivyo, kutaga mayai na uzito hupungua. Shida hii yaweza kusambaa hata kutoka mahali vifaranga huanguliwa hadi pale walipouzwa.
Tylosin19 ndio dawa inayoweza kutibu magonjwa ya mapafu. Kiasi cha 35mg ya tylosin hutosha
kuku mmoja (kiwango hiki hufaa kuku na hata vifaranga) dawa hii husimamisha madhara kutokana
na magonjwa ya mapafu. Tibu kuku kila baada ya miezi mitatu, waweza kutekeleza kwa wakati
mmoja wa kutoa kinga na kuangamiza minyoo. Tylosin hupatikana kwa pakiti ndogo ya 4gm.
Waweza kutayarisha dawa hii kwa kutumia maji na 35gm ya tylosin (gramu nne kwa vikombe viwili
vya maji), kiasi hiki chaweza kutolewa kwa vitone kwa kila kuku.


KWA UFUPI (SUMMARY)

Kabila za Kuku

Si rahisi kupata kabila halisi (pure breed) au kizazi halisi (pure line) za kuku wa kienyeji kutokana na mwingiliano wa vizazi kati ya aina mbalimbali za kuku hao. Lakini hata hivyo baadhi ya kuku wa kienyeji wanaweza kutambuliwa kutokana na maumbile yao kwa mfano

1. Kuchi

Warefuna wenye kusimama mgongo ukiwa wima
Wana manyoya machache mwilini na vilemba vyao ni vidogo
Majogoo huwa na wastani wa kilo 2.5 na mitetea kilo 1.8
Mayai gram 45

2. Ching'wekwe (Umbo dogo)

Hupatikana zaidi Morogoro na umasaini
Majogoo kilo 1.6
Mitetea kilo 1.2
Yai gram 37
kuku hawa wanafaa sana kwa biashara ya mayai kwa kuwa hutaga mayai mengi sana.

3. Umbo la Kati

Majogoo kilo 1.9
Mitetea kilo 1.1
Mayai gramu 43
Hukua upesi na hupata kinga upesi baada ya kuwachanja dhidi ya ugonjwa wa Mdondo (New Castle)

4. Singamagazi

Hupatikana zaidi Tabora
Majogoo wana rangi ya moto na mitetea rangi ya nyuki
Majogoo kilo 2.9
Mitetea kilo 2
Mayai gramu 56

5. Mbeya

Wanapatikana Ileje Mbeya na asili yao ni Malawi
Mjogoo kilo 3
Mitetea kilo 2
Mayai gramu 49
Uwezo wao wa kuatamia mayai na kuangua ni mdogo sana ukilinganisha na kuku wengine

6. Pemba

Maumbo ya wastani na miili myembamba
majogoo kilo 1.5
mitetea kilo 1
mayai gramu 42

7. Unguja

Hawatofautiani sana na wa Pemba
Vilemba vyake ni mchanganyiko- vidogo an vikubwa
Majogoo kilo 1.6
Mitetea kilo 1.2
Mayai gramu 42

SIFA ZA KUKU WA KIENYEJI

Wastahimilivu wa Magonjwa
Wana uwezo wa kujitafutia chakula
Huatamia, kutotoa na kulea vifaranga
Wanastahimili mazingira magumu(ukame, baridi n.k)
Nyama yake ina ladha nzuri

KATIKA KUWAENDELEZA KUKU WA KIENYEJI NI VYEMA

Wajengewe nyumba bora
Wapewe kinga dhidi ya ugonjwa wa Mdondo (New Castle), Ndui (Fowl Pox) pamoja na kinga ya minyoo.
Malezi bora ya vifaranga
Kuwapatia chakula cha ziada pamoja na maji ya kunywa ya kutosha.

NYUMBA BORA

Eneo inapojengwa nyumba au banda la kuku liwe
Linafikika kwa urahisi
Limeinuka juu pasituame maji
Pasiwe na pepo zinazovuma
Vifaa kama miti, nyasi, makuti, fito, udongo mabanzi ya miti, cement, mabati n.k
Sifa za Nyumba Bora ya Kuku
Paa imara lisilovuja
Kuta zisiwe na nyufa
Sakafu isiwe na nyufa
Madirisha ya kutosha kupitisha hewa
Iwe na mlango wa kuingia kufanya usafi
Iwe na ukubwa (nafasi) unaolingana na idadi ya kuku. Wastani wa kuku 10-15 kwa mita moja mraba
Mambo muhimu ndani ya nyumba
Chaga za kulalia kuku
Sakafu iwekwe maranda (wood shavings), makapi ya mpunga, n.k
Viota vya kutagia mayai sentimita 35x35x35 na idadi ya viota iwe nusu ya idadi ya kuku waliofikia hatua ya kutaga na viwekwe sehemu iliyojificha (faragha)

UATAMIAJI WA MAYAI

Kuna njia 2
Njia ya kubuni (incubators)
Asili
Kumuandaa kuku anayeatamia
Weka maranda au majani makavu ndani ya kiota
Anapokaribia kuatamia toa mayai ndani ya kiota pamoja na maranda, hakikisha mikono haina manukato
Nyunyiza dawa ya kuua wadudu (viroboto, utitiri n.k) ndani ya kiota, pia mnyunyizie dawa kuku anayetarajia kulalia mayai
Rudisha mayai kwenye kiota ili kuku aanze kuatamia
Kwa kawaida kuku hulalia mayai yake kwa muda wa siku 21 ndipo huanguliwa

ULEAJI WA VIFARANGA

 

Kuna njia mbili
Njia ya kubuni
Njia ya asili
Njia ya ASILI
Kuku mwenyewe hutembea na vifaranga akivisaidia kutafuta chakula. Ni vizuri kumtenga kuku mwenye vifaranga katika chumba chake pekee ili vifaranga wasishambuliwe na kuku wengine hali kadhalika kuwalinda na wanyama na ndege wanaoshambulia vifaranga.

Njia ya KUBUNI

Vifaranga huwekwa kwa pamoja kwenye chumba maalum na kupatiwa joto maalum, chakula pamoja na maji. Tumia taa ya kandili (chemli), umeme au jiko la mkaa na hiyo taa iweke kwenye mzingo(mduara) walipo vifaranga. Pia kuna kifaa kinaitwa Kinondoni Brooder ni kizuri kwa kutunzia vifaranga. Kwa kutumia kifaa hiki kuku wanaweza kunyang'anywa vifaranga vyao mara tu baada ya kutotoa na kuviweka kwenye hii brooder na hao kuku wakaachwa bila vifaranga vyao, baada ya majuma matatu au manne, kuku hao huanza tena utagaji na kuendelea na uatamiaji hadi kutotoa tena. Kwa mtindo huu kuku anaweza kutotoa mara 5-6 badala ya kama ilivyo sasa mara 2-3 kwa mwaka. Vifaranga vikae ndani ya brooder majuma 3-4 na baadaye fungua milango ya brooder kuruhusu vifaranga vitoke na kuzungukazunguka chumbani bila kuvitoa nje kw kipindi cha mwezi mmoja au zaidi kutegemeana na mazingira.

KULISHA KUKU WA KIENYEJI

Kuku mkubwa huhitaji gramu 120 za chakula kwa siku, ni vizuri kuku wanaofugwa huria (free range) kupatiwa chakula cha ziada gramu 30 kila siku nyakati za jioni.
Kuku walishwe
Mizizi-mihogo, viazi vitamu, mbatata, magimbi, n.k
Nafaka-mahindi, Mpunga, Mtama, Ulezi na Pumba za nafaka zote
Mboga-Mikundekunde, nyanya, milonge, majani ya mapapai
Matunda-Mapapai, maembe, n.k
Mbegu za Mafuta-Karanga, ufuta, mashudu ya pamba, alizeti, n.k
Unga wa dagaa
Maji

KUCHANGANYA CHAKULA CHA KUKU

Pumba………….kilo20
Mashudu ya Pamba n.k…kilo 3
Dagaa iliyosagwa………kilo 1
Unga wa majani uliokaushwa kivulini na kusagwa……..kilo 2
Unga wa Mifupa ……….kilo 0.25
Chokaa ya mifugo ……..kilo 0.25
Chumvi……………………gramu 30
Vichanganyio/Premix…gramu 25

KUPANDISHA

Uwiano wa mitetea na jogoo ni mitetea 10-12 kwa jogoo mmoja
Sifa za mtetea ni mkubwa kiumbo, mtagaji mayai mengi, muatamiaji mzuri na mlezi wa vifaranga
Sifa za jogoo ni awe mkubwa kiumbo, miguru imara na yenye nguvu, mrefu, upanga/kilemba kikubwa, awe na uwezo wa kuitia chakula mitetea na awe na tabia ya kupenda vifaranga
Jogoo huanza kupanda akiwa na umri wa miezi 7-10 na kuendelea hadi miaka mitatu na asipande watoto wake
Mitetea huanza kutaga wakiwa na miezi 6-8

MAGONJWA YA KUKU

1. Mdondo/New castle
Virus vinavyosababisha ugonjwa huu huenezwa kwa hewa

Dalili

Kuhalisha choo cha kijani na njano
Kukohoa na kupumua kwa shida
Kupinda shingo kwa nyuma
Kuficha kichwa katikati ya miguu
Kukosa hamu ya kula na kunywa
Idadi kubwa ya vifo hadi 90%

Kinga

Chanjo (New Castle vaccine) kwa mpango wa siku 3, wiki 3, miezi 3
Epuka kuingiza kuku wageni
Choma au fukie mizoga ya kuku waliokufa kwa ugonjwa
Zingatia usafi wa mazingira

NDUIYA KUKU/ FOWL POX

Virus huambukizwa kupitia jeraha au mbu

Dalili

Vidonda vyenye utando wa kahawia/purple kwenye sehemu zinazoonekana
Kukosa hamu ya kula
Vifo vingi

Kinga

Chanja vifaranga wanapofikia mwezi 1-2 kwa kutumia chanjo ya Fowl pox vaccine
Epuka kuingiza kuku wageni
Zingatia usafi wa mazingira

HOMA YA MATUMBO/FOWL TYPHOID

Kuharisha kinyesi cha kijani na nyeupe
Kuku hukosa hamu ya kula
Kuku hukonda
Vifo hutokea kidogo kidogo kwa muda mrefu
Kinyeshi hushikamana na manyoya

Tiba

Dawa aina ya antibiotic, sulfa na vitamini
Kinga

Usafi

Fukia mizoga
Usiingize kuku wageni
Chinja kuku wote mara ugonjwa huu ukiingia na safisha banda, pia pumzika kufuga kwa miezi 6

MAFUA YA KUKU/INFECTIOUS CORYZA

Hutokana na bakitelia na hushambulia hasa kuku wakubwa

Dalili

Kuvimba uso
Kamasizilizochanganyikana na usaha unaonuka
Macho huvimba na kutoa machozi na pengine upofu
Hukosa hamu ya kula
Mbawa huchafuka na kutoa harufu mbaya
Tiba
Dawa za Antibiotic, sulfa na vitamini

KUHALISHA DAMU/COCCIDIOSIS

Husababishwa na vijidudu vya Protozoa

Dalili

Kuharisha damu
Manyoya husimama
Hulala na kukosa hamu ya kula

MINYOO

Dalili

Kunya minyoo
Hukosa hamu ya kula
Hukonda au kudumaa
Wakati mwingine hukohoa
Tiba
Dawa ya minyoo/Pipeazine citrate kila baada ya miezi mitatu

WADUDU

Viroboto, chawa, utitiri

Dalili

Kujikuna na kujikung'uta
Manyoya kuwa hafifu
Rangi ya upanga kuwa hafifu
Ngozi kuwa nene, ngumu na yenye magamba yanayodondoka kama unga
Kuzuia
Ziba mipasuko sakafuni na kwenye kuta za banda
Fagia banda mara mbili kwa wiki
Nyunyiza majivu au chokaa mara moja kwa wiki mara baada ya kufagia
Choma masalia ya mayai yaliyoanguliwa
Nyunyiza dawa kwenye viota
Weka maranda, majani makavu, makapi ya mpunga ya kutosha sakafuni ndani ya banda la kuku
Fuata kanuni za chanjo
Tenga kuku wagonjwa wakae mbali na kuku wazima

UPUNGUFU WA VIINI LISHE KWENYE CHAKULA

Dalili

Kuku hupungua damu, uzito na kudumaa
Mifupa huwa laini na kutokuwa imara
Hutaga mayai yenye gamba laini na madogo
Huwa na manyoya dhaifu







Related Posts

UFUGAJI BORA WA KUKU WA KIENYEJI
4/ 5
Oleh

Subscribe via email

Like the post above? Please subscribe to the latest posts directly via email.